Utangulizi
Kimvuli kinatokana na eneo la umbo ambalo limezuia mwanga kupita, mara zote kimvuli cha mtu au kitu kinatenda matendo yale yale yanayotendwa na kitu kilichosababisha kimvuli hicho. Hivyo hivyo watu wengi tunaishi maisha yetu kama vimvuli kwa kutenda yaleyale yanayotendwa na wenzetu.
Naamini wengi wetu tutakuwa mashuhuda, mara kadhaa tulipohitaji kusoma kozi fulani, tuliauliza watu tukasome kitu gani, mara nyingi sana watu hawa walitushauri tukasome walichosomea wao. Wakati mwingine tumelazimika kusomea walichosomea wazazi au ndugu zetu nk.
Hatujaishia katika masomo tu, wengine tumeiga hata shughuli za kufanya kwa hisia kuwa wanaofanya shughuli hizo wamefanikiwa. Wengine tumeiga tabia za wazazi wetu na watu wetu wa karibu bila kujali kuwa ni tabia nzuri au mbaya. Mfano, mtu aliekulia katika maisha ya mzazi wa kiume kumpiga mzazi wa kike, haitashangaza akikutwa anampiga mzazi mwenzie.
Mambo haya na mengine mengi, yamesababisha wengi wetu tuishi kama vimvuli. Maisha tunayoishi leo hii ni maisha yaleyale walioishi au wanayoishi baadhi ya watu waliotuzunguka. Zipo sababu nyingi sana zinazochangia tuendelee kuishi kama vimvuli kama ifuatavo hapa chini.
Kwanini tunaisha kama kimvuli?
Kila mwanadamu anapozaliwa inaaminika kuwa ubongo wake unakuwa hauna taarifa nyingi. Ndio maana ni rahisi sana mtoto kushika moto au kumkimbilia nyoka sababu hana taarifa kuhusu moto wala nyoka. Hali hii inawafanya watoto wengi kuwa huru na kutokuwa waoga, wanaweza kufanya lolote wanalojisikia kufanya.
Mara baada ya kushika moto, ubongo wa mtoto unapata taarifa ya maumivu kutoka katika milango yake ya fahamu. Mtoto anaweza kuachia moto na asiushike tena hata watu wasipokuwepo karibu, hii inatokana na sababu kuwa anayo taarifa kuhusu nini kitatokea akiushika tena moto ule.
Kila mtu ana viuongo vya fahamu kama vile masikio, ulimi, ngozi, macho,na pua. Viungoa hivi mara mtoto anapozaliwa vinaanza kazi ya kukusanya taarifa mbali mbali kkatika mazingira yanayomzunguka mtoto. Mtoto anasikia wazazi wakiongea, anaona wakipigana, akipewa dawa anatema baada ya kuhisi uchungu, anaona wazazi wakisali nk.
Taarifa hizi hupokelewa na viungo vya fahamu na kufikishwa katika ubongo wa mtoto. Ubongo wa mtoto unatafakari taarifa iliyopokelewa na kulazimisha sehemu za mwili zinazohusika na taarifa hizo kutenda kulingana na taarifa iliyopokelewa. Taarifa hizi zikipokelewa na ubongo wa mtoto kwa muda mrefu, zinajenga imani na matendo ya mtoto. Tuangalie mfano ufuatao.
Nini chanzo cha tabia zetu?
Tabia ni matendo ambayo tunayafanya mara kwa mara au kwa kujirudiarudia. Tabia za mwanadamu zinaweza kujengwa kutokana na taarifa ambazo binadamu anazipokea mara kwa mara. Tuangalie mfano ufuatao.
TAARIFA- MILANGO YA FAHAMU- UBONGO- MAWAZO- HISIA-MUHEMKO- MATENDO- MATENDO YA KUJIRUDIA.
Taarifa zote zinazotokana na mazingira yanayotuzunguka, hupokelewa na milango ya fahamu kama macho kwa kuona, masikio kwa kusikia, ulimi kwa kuonja, ngozi kwa kuhizi na pua kwa kunusa. Taarifa zote hizi zinasafiri kupitia milango ya fahamu na kufika katika ubongo wa mwanadamu.
Ubongo wa mwanadamu ndio injini ya kila tendo analotenda mwanadamu, mara zote mwanadamu hutenda kutokana na kile alichokifikira katika ubongo wake. Ubongo hutafakari kila taarifa inayoingia kichwani na kutoa muongozo wa nini kifanyike. Ni kama vile mtu akiona nyoka ghafla, anaweza shituka na kukimbia au kumfuata na kumuua nyoka huyo.
Matendo mengi tunayotenda ni matokeo ya kile tunachokiwaza katika ubongo wetu kutokana na taarifa tulizonazo. Ndio maana mtu aliegongwa na nyoka, akiguswa na jani huushituka sana sababu ndani ya ubongo wake kuna taarifa ya maumivu ya kung’atwa na nyoka. Tofauti kabisa na mtu ambaye hajawahi patwa na tukio hili.
Ufafanuzi
Taarifa hupokelewa na viuongo vya fahamu na kufika katika ubongo.
Ubongo unatafsiri taarifa hizo na kutengeneza mawazo.
Mawazo ni matokeo ya ubongo kutafakari taarifa ulizopokea, taarifa hzzi zikiendelea kupatikana kwa muda zaidia, mawazo huongezeka pia na kuzalisha hisia.
Hisia ni zao la mawazo mengi au ukubwa wa mawazo yaliyotokana na taarifa fulani iliyofika katika ubongo. Kama taarifa hiyo itaendelea kuwepo zaidi, mawazo yataongezeka na hisia zitaongezeka na kuzaa muhemko.
Muhemko ni hisia kali zinazolazimisha tendo kufanyika kulingana na taarifa, mazo na hisia. Hisia zinapoongezeka, muhemko huwa mkubwa na mtu kushindwa kujizuia, hivyo anatenda tendo kulingana na muhemko ulivyo mtuma.
Tendo, tendo ni zao la mihemko, kwa kawaida baada ya kuzidiwa na muhemko na kufanya tendo. Uzuri au ubaya wa tendo hupokelewa tena kama taarifana kufika katika ubongo na kuhifadhiwa.
Tabia hutokana na matendo yakujirudia na kisha kuzoeleka, tunapokuwa hatuna kazi ya kufanya au ubongo hauna taarifa za kufanyia kazi, ubongo unatabia ya kutukumbusha kuhusu matendo tuliyofanya nyuma na kusababisha kurudiwa kwa matendo hayo. Tunaporudia mara kwa mara tunazoea na kuwa tabia zetu.
Tabia na maisha ya kila siku
Katika maisha ya kila siku tunapokea taarifa nyingi sana, tangu tukiwa watoto, tumesikia na kuona mengi kwa muda mrefu. Mambo tunayosikia na kuyaona kwa muda mrefu, hujenga imani juu ya mambo hayo na kuanza kuathiri matendo yetu binafsi ya kila siku. Mfano, sio rahisi kwa mtoto kuwa mkristu angali amezaliwa ktk familia ya kiislamu, hivyohivyo kwa muislamu kuwa mkristu.
Mazingiria tuliyokulia tukiona wazazi na ndugu zetu wakiswali au kusali kwa muda mrefu, hutujengea thamani na imani juu ya matendo hayo na kuanza kuyaishi. Tukiwa watoto tulipelekwa Sunday schools, madrasa, wapo waliolelewa kwa matambiko nk. Wote hawa hawawezi kuishi tofauti na jamii au mazingira yanayowazunguka au yaliyowazunguka kwa muda mrefu wa maisha yao. Tunapowaona watoto wadogo kabisa wanatukana matusi mazito bila hata kujua maana ya matusi hayo, ni ishara ya aina za taarifa mtoto huyu anazipokea katika mazingiria yanayomzunguka.
Taarifa ktk jamii ya leo
Wingi na urahisi wa upatikanaji wa taarifa leo hii, unachangia kwa kiasi kikubwa sana watu kuishi maisha ya kuiga yale wanayoyaona, kusikia na kuhisi. Kuna ushahidi wa kutosha juu ya mmong’onyoko wa maadili katika jamii unaotokana na taarifa za mitandao. Mbali na kuishi na watu wanaotupatia taarifa mbalimbali, mitandao ya kijamii, redio, Tv na magazeti vimekuwa chachu kubwa ya mabadiliko mengi chanya na hasi katika jamii zetu.
Urahisi na upatikanaji wa taarifa katika jamii kila siku, kumerahisisha sana uwepo wa taarifa nyingi zisizo sahihi au taarifa sahihi kuwasilishwa katika namna isiyo sahihi. Ndio maana leo hii watu wengi wanateseka sana kuhusu neno mafanikio, mahusiano nk kutokana na taarifa zilizopo ambazo hazipo sahihi. Jamii inawaaminisha watu kuwa mafanikio ni kuwa na magari, majumba na mali nyingi, hivyo kila tunaotaka kufanikiwa tunatafuta vitu vilevile.
Wasichana wanaona na kusikia Dada na kaka zao wakiolewa wakiwa umri fulani, basi inakuwa ni mazoea na kila mtu anapigania kuoa au kuoelewa mara tu anapofikia umri huo. Sababu waliosomea mambo ya bank wanaonekana kuishi maisha mazuri, jamii inaamini kuwa masomo hayo ndio masomo ya watoto wao kusoma bila kujali uwepo wa ajira hizo.
Ubongo ni shamba letu la thamani
Shamba lolote linaweza kuotesha chochote kilichopandwa, lakini hata lisipopandwa kitu, litajiotea chochote kinachowezekana kuota katika shamba hilo. Kama tukipanda mahindi na tusipokuja kupalia, tukija kuvuna tutavuna mahindi na magugu yasiyoliwa. Ili tuweze kuvuna mahindi pekee ni lazima tupalie baada ya kupanda.
Maisha ya kila siku yamepanda mbegu nyingi sana katika shamba letu ubongo kwa milango yetu ya fahamu kusikio, kuona, kuhisi, kunusa taarifa mbalimbali. Na baada ya muda taarifa hizi zinazoeleka na kuaminika nasi na kuathiri matendo yetu moja kwa moja. Wengi tumejikuta tukikosa uhuru wa kuwa vile tunavyotaka kutokana na taarifa tulizonazo kutoka katika jamii zetu.
Kuna muda ambao tulipokea taarifa mbaya hivyo kupanda mbegu mbaya katika ubongo wetu na kupelekea kuwa na tabia au matendo yasiofaa kwa jamii au kwetu sisi binafsi na wenzetu. Kuhusu jamii inasema nini kuhusu matendo yetu inaweza kuwa sio shida, shida ni pale ambapo, sisi wenye tunalazimika kufanya mambo ambayo hata hatupendi kufanya ila tunalzimishwa na mazingira.
Wapo watu wengi wanateseka sana leo hii kuishi maisha yao, sababu tu wanawaza jamii itamuonaje, au analinganisha anachotaka kufanya na yale ambayo ameshayasikia. Kwa kuwa sauti ya tunayosikia huwa ni kubwa sana na zenye kufifisha sauti zetu za ndani, basi tunaamua kuachana na sauti zetu za ndani na kufuata taarifa zilizopo. Hii ndio sababu kubwa inayotufanya tuishi kama vimvuli vya watun wengine, kwa kuiga matendo ya taarifa tunazosikia au kuona.
Palizi ni muhimu kwa mavuno bora shambani
Kama ilivyo shamba, ubongo wetu umeshaokota taarifa nyingi sana, nzuri na mbaya. Ni jukumu letu kuhakikisha tunaweza kuchambua taarifa tunazozipokea, kutabiri matokeo yake baadae na kufanya maamuzi ya kupalilia mashamba yetu ya ubongo kwa kuondoa taarifa mbaya na kubakisha taarifa nzuri zinazotufaa.
Kuna wakati nikiwa nafundisha, niliwauliza washiriki kwanini wanafikiri wao ni masikini? Wengi walinijibu kuwa Mungu ndie alieamua wao kuwa masikini na siku akiamua wawe matajiri watakuwa. Hii haijatokana na kingine zaidi ya mafundisho au taarifa walizonazo kuhusu Mungu. Lakini, taarifa hii inafifisha uwezo wa watu kujituma katika mambo muhimu na hata kuwafanya wakeshe tu wakiomba bila kufanya kazi.
Taarifa kama hii hufifisha uwezo wa mwanadamu kuishi maisha ya furaha, hivyo haiwezi kuwa taarifa nzuri kwakuwa haichochei matendo mazuri bali matendo yasiyo sahihi. Mara nyingi tunapofanya matendo yasiyo sahihi, huwa tunafanya kwaajili ya kufurahisha jamii zaidi kuliko sisi wenyewe. Ninakumbuka wakati nikiwa chuo ST. Joseph College of Engeneering, nilikuwa navutiwa sana na maandiko ya ukutani yaliyosema, Kazi na sala. Taarifa hii inachochea watu kufanya kazi pamoja na kusali ili kujiondoa katika hali waliyopo.
Tunahitaji kuwa makini sana na taarifa tunazozipokea mara kwa mara katika maisha yetu na kama tayari tulishapokea taarifa mbaya basi tuanze kuzifuta kwa kupalilia bongo zetu kwa kuondoa taarifa zisizotufaa. Taarifa mbaya huketa matendo au tabia mbaya na taarifa nzuri huleta matendo au tabia nzuri. Tunaweza badilisha tabia au matendo yetu kwa kubadilisha taarifa tunazoruhusu kuingia na kufanyiwa kazi na bongo zetu.
Mahusiano ya tabia na malengo yetu
Wengi wetu tunatoka utotoni mpaka katika utu uzima wetu tukiwa tumeshakopi tabia nyingi sana hatari kwa maisha yetu na hasa malengo yetu. Wengi tunapanga malengo katika kipindi cha utu uzima. Tusiichokijua mara nyingi tunapanga malengo kulingana na uwezo wetu wa kufikiria ambao tayari uumeathiriwa na taarifa nyingi tulizobeba katika jamii.
Mara nyingine tunafanikiwa kupanga malengo mazuri na mapya kabisa lakini tunashindwa kuyatekeleza kulingana na malengo yetu kutofautina na tabia zetu. Mfano, tunapnga malengo kuwa mwalimu bora na maarufu tunaonpendwa na wazazi na watoto. Lakini kushuhudia kwa muda mrefu watoto wakipigwa na kufokewa ikiwemo sisi wenyewe tukiwa watoto. Tunabeba tabia hizo, tukifanikiwa kuwa walimu tunaishia kufungwa jela kwa kuumiza watoto au kukosa kazi kwa sababu ya tabia hizo hatarishi.
Mtu anayeamua kufungua biashara ya kuuza vilevi na yeye anatabia ya ulevi, ni rahisi sana biasharra yake kuteseka kutokana na tabia zake na hasa akishindwa kutambua tabia anazohitaji ili kufikia malengo ya biashara yake. Tusichokifahamu ni kuwa tumepanda malengo ambayo yanahitaji tabia tofauti na zile ambazo tayari mazingira yametujengea. Ili tuweze kutimia malengo yetu, tunahitaji kujua tabia zinazofaa kwa malengo hayo kutimia, pamoja na kuanza kujijengea tabia mpya zinazofanania malengo au ndoto zetu.
Njia rahisi ya kujenga tabia mpya
Kwanza tunahitaji kujua chanzo cha tabia zetu mbaya ambacho mara zote ni taarifa tulizisikia au kuona mara kwa mara. Pili ni kujitambua na kuishi kwa malengo. Tunapotambua malengo yetu hutusaidia kujua mambo mapya ya kufanya ambayo mengine hayaendani na tabia zetu, hivyo kutulazimu kuachana na tabia zetu za sasa na kujijengea tabia mpya.
Ili kubadilisha tabia zetu zisizofaa tunahitaji kwanza kubadilisha taarifa tunazozipokea kila siku kutoka katika mitandao, majirani, ndugu na marafiki. Ndio maana watu hushauri hata ikibidi kubadili marafiki zetu, binti mwenye pepo la ngono, hata akiombewa na wachungaji wote duniani pepo haliwezi toka kama ataendelea kuwa na marafiki walewale, au kusikiliza na kuona taarifa za ngono zilezile kupitia simu yake baada ya maombi.
Tatu, tujitahidi sana kuishi matendo yetu mapya tunayoyataka. Kumbuka matendo haya tukiyafanya mara kwa mara, yanazoeleka na kuwa tabia zetu. Kujitambua na kupanga malengo, kunatusaidia sana kubadilisha tabia na kujijengea tabia mpya kwa kutulazimisha kujiweka katika mazingira yanayotupatia taarifa zinazofanania ndoto au malengo yetu. Hata wagonjwa wa dawa za kulevya, hulazimika kupelekwa rehabu ili kuwabadilishia mazingira yao ili kuwasahaukisha taarifa walizozea kuzipata wakiwa vijiweni.
Maisha kama kivuli au maisha ya kuiga, huinyima dunia au jamii mawazo mapya. Waliogundua umeme, usafiri wa anga na majini, matumizi ya Kopmpyuta nk. Wangeishi kwa kuiga wasingeweza kuleta mambo mapya katika jamii zao na dunia kwa ujumla. Kila mtu anauhuru wa kufikiri na kutenda, na wengine wakaiga mifano yao kama matokeo yao yatakuwa mazuri. Kwahiyo kuiga sio tatizo, tatizo ni pale ubunifu wetu binafsi unapozuiwa na mazoea. Tujifunze kwa tunayoyaona na kusikia, lakini yasiwe sheria kwetu hata kushindwa kuonesha uwezo wetu na kuiletea dunia, jamii na familia zetu mambo mapya.
Asante kwa kusoma
Imeandaliwa na Mwalimu David
Learning & growth Partner.
Write a comment
Juma Aweso Salum (Tuesday, 29 March 2022 13:32)
Kwanza kabisa nipongeze niandiko lenye ujumbe mnzito sana hasa kwa vijana na pia muendelee kwa ajili ya kukomboa fikra za vijana